WAKENYA NA WATANZANIA WALIFARIKI MECCA
25/9/2015
Mahujaji watatu
kutoka Kenya ni miongoni mwa watu 717 waliofariki baada ya mkanyagano
kutokea karibu na mji wa Mecca, Saudi Arabia, afisa wa serikali ya Kenya
amesema.
Bw Washington Oloo, afisa wa wizara ya mashauri ya
kigeni anayehusika na masuala ya Wakenya wanaoishi ng’ambo amesema
Mkenya mwingine mmoja aliumia na amelazwa hospitalini. Mahujaji wanane
bado hawajulikani waliko.Nchini Tanzania kiongozi mmoja wa Kiislamu nchini humo amesema wamethibitisha kuwa raia wanne wa Tanzania walifariki katika mkasa huo uliotokea Alhamisi.
"Nimepokea taarifa za majeruhi miongoni mwa mahujaji wetu wa Tanzania na baadhi ya majeruhi nimeonana nao mara baada yao kuruhusiwa kuondoka hospitalini,” amesema mufti wa Tanzania Sheikh Abu Bakari Zuberi aliye Mecca, kupitia taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari.
"Katika kipindi hiki cha taharuki kubwa, tunafanya mawasiliano na wizara husika hapa Saudi Arabia."
Alisema maafisa wa Saudia bado wanaendelea kutambua uraia wa waliofariki.
Mkanyagano ulitokea eneo la Mina mahujaji walipokuwa wakielekea kwenye nguzo za Jamaraat.
Nguzo hizo zimo katika eneo ambalo inaaminika Nabii Ibrahim alijaribiwa na shetani.
Idara ya ulinzi wa raia Saudi Arabia imesema mkanyagano huo ulitokea pale kulipotokea "ongezeko la ghafla" la watu waliokuwa wakielekea kwenye kwenye nguzo hizo.
Waziri wa afya wa Saudi Arabia Khaled al-Falih amesema mkanyagano huo ulitokea kwa sababu mahujaji walikosa kufuata maagizo.
"Wengi wa mahujaji huenda bila kufuata ratiba iliyowekwa," amesema.
No comments:
Post a Comment